Dei Verbum
Dei Verbum (katika Kilatini maana yake ni "Neno la Mungu") ni jina fupi la hati ya kidogma ya Mtaguso wa pili wa Vatikano kuhusu ufunuo wa Mungu katika imani ya Kanisa Katoliki.
"Dei Verbum" ni maneno mawili ya kwanza ya hati hiyo iliyotolewa kwa lugha ya Kilatini.
Maaskofu na makasisi 2344 kati ya waliohudhuria mtaguso huo walikubali hati hiyo wakati 6 tu waliipinga, halafu Papa Paulo VI aliitangaza kama mafundisho ya kanisa tarehe 18 Novemba 1965. Hutazamwa kuwa kati ya hati muhimu zaidi za mtaguso.
Mkazo wa hati hiyo ni mafundisho juu ya ufunuo wa Mungu katika Historia ya Wokovu ya Agano la Kale na Agano Jipya, ambao ulikamilishwa na Yesu Kristo na kukabidhiwa kwa Kanisa ili liutunze katika mapokeo yake, liufafanue kwa mamlaka ya maaskofu (Ualimu wa kanisa) kwa kutegemea hasa Maandiko matakatifu ambayo yanatakiwa kushika tena nafasi inayostahili katika maisha ya Wakristo wote.
Sababu za kutoa Dei Verbum
Katika Kanisa Katoliki tangu zamani sana zilisisitizwa liturujia na sakramenti.
Ibada hizi ziliendeshwa hasa kwa Kilatini hata baada ya lugha hiyo kufa katika karne za kati.
Hivyo waamini walikuwa hawaelewi masomo ya Biblia kwa kukosa tafsiri yake katika lugha zao.
Kuanzia karne XII tafsiri za Biblia zilianza kupatikana kwa juhudi za watu ambao kwa kawaida hawakukubaliwa na maaskofu wa kanisa kwa jinsi walivyojaribu kuifafanua kinyume cha mapokeo.
Baadaye ulipobuniwa uchapishaji huko Ulaya walikuwa hasa wataalamu wa Kiprotestanti kama Martin Luther waliotunga tafsiri zilizosambazwa kote, wakati uongozi wa Kanisa Katoliki haukukubali usahihi wa kazi hiyo, hivyo Biblia ikazidi kubaki pembeni mwa maisha ya Wakatoliki wengi.
Hivyo kabla ya Mtaguso wa pili wa Vatikano Wakatoliki kwa jumla badala ya kuipenda Biblia walikuwa wakiogopa kupotoshwa nayo kadiri ya onyo la 2Pet 3:16.
Kumbe hati hiyo ilipotolewa baada ya majadiliano na marekebisho mengi imelirudishia Kanisa lote Maandiko Matakatifu.
Baada ya hapo Wakatoliki wataalamu wa Biblia wamefanya kazi kubwa sawa na wenzao Waprotestanti.
Waseminari na watawa wengi wamefundishwa sana Neno la Mungu, na hata walei wameanza kulifurahia.
Matunda yake yamepatikana tayari katika uzima mpya unaoonekana katika mifumo ya Kiroho, vyama na jumuia mbalimbali.
Sura ya kwanza
Baada ya dibaji, inayotamka nia ya kufuata nyayo za mitaguso iliyotangulia, sura ya kwanza inahusu ufunuo wa Mungu.
Ni kwamba haiwezekani kuelewa Biblia mbali na Historia ya Wokovu, kwa sababu si kitabu kilichoandikwa leo kwa ajili ya msomaji binafsi, bali kilipatikana zamani Mungu alipojifunua hatua kwa hatua kwa taifa zima la Israeli.
Sura ya pili
Sura ya pili inafundisha jinsi ufunuo huo, uliokamilika zamani za Yesu, unavyowafikia watu wa leo, yaani kwa njia ya Mapokeo ya Mitume yakiwa na Maandiko Matakatifu ambayo kwa pamoja ni hazina takatifu ya Neno la Mungu, si chemchemi mbili tofauti.
Hazina hiyo imekabidhiwa kwa Kanisa ambalo linaweza kuifafanua rasmi kwa njia ya Ualimu wake.
Basi, Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Ualimu wa Kanisa yameshikamana na kuunganika kiasi kwamba moja haliwezi kusimama bila ya mengine.
Sura ya tatu
Baada tu ya kuelewa hayo inawezekana kukabili Biblia yenyewe kwa kuzingatia jinsi Roho Mtakatifu alivyovuviwa juu ya watunzi wake.
Hao walifanya kazi kama waandishi wowote, lakini vitabu vilivyopatikana vinafundisha tu kwa hakika na bila ya kosa ule ukweli ambao Mungu alitaka uandikwe kwa wokovu wetu.
Mtaguso ulisistiza kuwa lengo la Biblia si kufundisha ukweli wowote (k.mf. wa sayansi) bali ule unaohusu wokovu: katika hilo haiwezi kukosea.
Ni kwamba Biblia mwandishi wake hasa ni Mungu, lakini yeye alijieleza kwa njia ya watu, tena kwa namna ya kibinadamu.
Basi, mtu akitaka kumuelewa anapaswa kuelewa kwanza watunzi wa Maandiko matakatifu walitaka kusema nini, akizingatia pia mitindo ya uandishi waliyoitumia.
Utaalamu huo ni muhimu ingawa hautoshi, kwa sababu ni lazima bado kuzingatia umoja wa Biblia nzima, Mapokeo ya Kanisa na kweli za imani.
Sura ya nne
Baada ya kuona habari za Biblia kwa jumla, sura ya nne inaeleza umuhimu wa Agano la Kale kwa Wakristo pia, kwa kuwa linashikamana na Agano Jipya kama kitabu kimoja ambacho pande zake mbili zinahitajiana.
Sura ya tano
Sura ya tano inaeleza juu ya Agano Jipya: kwanza ubora wake unaozidi vitabu vya Agano la Kale; halafu asili ya Kitume ya Injili nne ambazo tena zinapita hata Maandiko mengine ya Agano Jipya; mwishowe hakika ya kihistoria ya Injili hizo.
Hati hii imepokea pia mtazamo mpya uliosema Wainjili waliandika historia ya Yesu kwa kuchagua baadhi ya habari walizokuwanazo juu yake, kufupisha nyingine na kueleza upya nyingine kadiri ya mazingira, wakidumisha namna ya kuhubiri kwa lengo la kufanya wasomaji waweze kuamini, lakini bila ya kupotosha ukweli.
Habari zenyewe ziliwaelea kwa mwanga wa Roho Mtakatifu aliyelifikia Kanisa baada ya Kristo kufufuka ili kuliongoza kwenye ukweli wote.
Sura ya sita
Hatimaye sura ya sita inatoa maagizo kuhusu Maandiko Matakatifu katika maisha ya Kanisa.
Kwanza ziwepo juhudi mpya ili wote wapate lishe katika meza ya Neno la Mungu ambalo ni hai na lina nguvu.
Pia juhudi zifanyike ili waamini wapate Maandiko hayo katika lugha zao.
Wataalamu pamoja na kuyatafsiri wayafafanue na kuelimisha wengine.
Wale wote wanaotoa mafundisho ya imani katika ngazi zozote washikamane na Maandiko kwa kuyasoma pamoja na kusali ili Biblia iwe kiini cha mafundisho yao.
Waamini wote, hasa watawa, wanahimizwa kuisoma sana kwa sababu kutoijua ni sawa na kutomfahamu Kristo.