Dionysius Exiguus
Dionysius Exiguus (aliishi takriban 470 - 544) ni jina la mmonaki Mkristo aliyeishi mjini Roma mnamo mwaka 500 BK. Anajulikana zaidi kama mtaalamu aliyeanzisha hesabu ya miaka "baada ya Kristo".
Dionysio alikuwa mwenyeji wa Scythia (Romania ya leo) akawa mmonaki na kuhamia Roma alipoheshimiwa kwa sababu ya elimu yake. Alitafsiri maandiko mengi kutoka lugha ya Kigiriki mkwa Kilatini.
Aliandika pia vitabu juu ya hisabati na hasa namna ya kupigia hesabu tarehe ya Pasaka.
Anno Domini
Wakati wake ilikuwa jambo gumu kukadiria tarehe za kihistoria. Watu walitumia mahesabu mbalimbali. Wengi waliendelea na desturi ya zamani ya kutaja mwaka wa "konsuli" iliyokuwa cheo kikuu Roma mjini. Lakini makonsuli walibadilika kila mwaka ikawa utaratibu mgumu kwa kazi ya kihistoria. Wakristo wengi walifuata desturi ya Misri wakihesabu miaka tangu Diokletiano aliyekumbukwa kwa sababu mateso yake makali dhidi ya Wakristo. Lakini Dionysio hakupenda kukumbuka mtawala aliyedhulumu Wakristo. Hivyo alikadiria mwaka wa kuzaliwa kwake Yesu.
Hesabu hii inaitwa "anno Domini" yaani "katika mwaka wa Bwana (Yesu)" (anno= kilat. "mwaka"; Domini = Kilat. "Bwana"). Kifupi chake ni "AD".
Haijulikani jinsi alivyofikia hesabu hii. Leo hii inajulikana ya kwamba kadirio lake lilikuwa na kosa ndogo.
Uenezaji wa hesabu ya Dionysio
Mwanzoni hesabu ya Dionysio haikujulikana isipokuwa kati ya wataalamu wachache. Wafalme wa Ulaya walipendelea kuhesabu miaka ya utawala wao wakiiga mfano wa Waroma wa Kale.
Lakini kanisa katoliki lilianza polepole kutumia hesabu yake. Mnamo mwaka 1000 ilikuwa kawaida katika hati rasmi za Ulaya.
Kosa la Hesabu ya Dionysio
Hesabu ya Dionysio ina kosa la miaka kadhaa. Wakati wake Dola la Roma lilikuwa limeshakwisha katika Italia, Kaisari alikaa Bizanti au Roma ya Mashariki. Kumbukumbu za Roma yenyewe hazikutunzwa tena tangu miaka mingi. Leo hii wataalamu wengi hukubaliana ya kwamba kasoro la Dionysio ni takriban miaka 4 - 8; yaani mwaka halali wa kuzaliwa kwake Yesu ulikuwa kama miaka nne hadi nane kabla ya mwaka ambao tumezoea kuhesabu kama "1".
Wengi walijaribu kusahihisha kosa hili lakini habari kamili kabisa hazipatikani tena.