Kiongozi wa kiroho

Yohane Bosco alikuwa maarufu kama kiongozi wa kiroho wa vijana.

Uongozi wa kiroho (kwa Kiingereza: Spiritual direction) ni msaada ambao muumini anampa mwingine katika juhudi za kuimarisha uhusiano wake na Mungu au kustawisha maisha ya kiroho aliyonayo. Aliyeomba msaada huo anajieleza na kumshirikisha kiongozi wake mang'amuzi mema na mabaya aliyoyapata katika safari yake ya kiroho. Kiongozi anasikiliza na kutoa maswali ili kumfanya muumini ajielewe zaidi na hatimaye anaweza akampa maelekezo ya kufaa, bila kuishia katika msaada wa kisaikolojia.

Katika Kanisa Katoliki

Huo ni kati ya misaada ya nje iliyo muhimu zaidi ili kufikia ukamilifu wa Kikristo hivi kwamba unahitajika kwa jumla na katika hatua tatu za maisha ya kiroho.

Haja ya uongozi kwa jumla

Ingawa uongozi si wa lazima kwa utakatifu, ni njia ya kawaida ya maendeleo ya Kiroho.

Yesu alipounda Kanisa lake alitaka waamini wawe chini ya Mitume na waandamizi wao (Papa na maaskofu) upande wa nje, na chini ya waungamishi upande wa ndani, hao wakiwaelekeza kutoanguka dhambini na kusonga mbele katika maadili. Mtume Paulo alipoongoka, Bwana hakumfunulia mwenyewe mipango yake, bali alimtuma Damasko kwa Anania, ajue kwa njia yake yatakayompasa kuyafanya (taz. Mdo 9:6).

Mababu wa Kanisa walihimiza: “Fanya bidii sana na uangalifu mkubwa kabisa ili kumpata mtu ambaye aweze kukuongoza kwa hakika katika kazi uliyokusudia ya kuishi kitakatifu; umchague mtu anayeweza kuwaelekeza wenye mapenzi mema njia nyofu ya kumuendea Mungu… Ni kiburi kabisa kudhani huna haja na mashauri” (Bazili Mkuu). “Usijifanye mwalimu wako mwenyewe, la sivyo utapotea haraka sana” (Jeromu). “Kama vile kipofu asivyoweza kushika njia nyofu asipoongozwa na mtu, hakuna anayeweza kutembea bila kiongozi” (Augustino). Yohane Kasiano alisema mtu anayetegemea akili yake hatafikia kamwe ukamilifu wala hataweza kukwepa hila za Ibilisi; njia bora ya kushinda vishawishi vya hatari ni kuvifunua kwa kiongozi mwenye busara na mwanga. Kweli, mara nyingi inatosha kuvifunua kwa anayehusika ili viishe.

Hata katika karne za kati watakatifu waliendelea kusisitiza: “Anayejifanya kiongozi wake mwenyewe anajifanya mwanafunzi wa mpumbavu… Upande wangu natamka kuwa kwangu ni rahisi na ya hakika zaidi kuagiza wengi kuliko kujiongoza mimi tu” (Bernardo). Katika kuongoza wengine umimi wetu unatudanganya kidogo kuliko katika kujiongoza; na kama tungejua namna ya kutekeleza wenyewe yale tunayowaambia wengine, maendeleo yetu yangekuwa makubwa. “Bwana wetu, ambaye pasipo yeye hatuwezi kitu, hatamjalia kamwe neema yake yule ambaye, ingawa anaye mtu mwenye uwezo wa kumfundisha na kumuongoza, anapuuzia chombo hicho muhimu cha utakatifu, akidhani anajitosheleza na kuweza kwa nguvu zake kutafuta na kuona yanayofaa kwa wokovu wa milele… Aliye na kiongozi ambaye anamtii katika yote na kikamilifu, atalifikia lengo lake kwa urahisi na haraka sana kuliko kama akifanya peke yake, hata kama ana akili sana na vitabu vyenye hekima kuhusu mambo ya Kiroho… Kwa jumla, wale wote waliofikia ukamilifu wamefuata njia ya utiifu, isipokuwa kama kwa fadhili au neema ya pekee Mungu alimfundisha mwenyewe mtu mmojammoja asiyekuwa na wa kumuongoza” (Visenti Ferrer).

Hadi baadaye, mkazo ulikuwa huohuo: Fransisko wa Sales alionyesha hatuwezi kuamua kwa haki kesi zetu wenyewe, kutokana na aina ya kujipendea “ya siri na isiyotambulikana ambayo tusipoangalia vizuri hatuwezi kuivumbua; na waliopatwa nayo hawaijui wasipoonyeshwa”. Aliyekaa muda mrefu katika chumba ambacho milango na madirisha yake yamefungwa hatambui kuwa humo hewa imechafuka kwa kupumua, kumbe anayeingia anatambua mara. Sisi sote tunakubali kwamba kiongozi anahitajika ili kupanda mlima mrefu; bila shaka anahitajika zaidi ili kupanda hadi kilele cha ukamilifu, hasa kwa sababu tunapaswa kuepa hila za yule asiyetaka tupande. Alfonso Maria wa Liguori alitaja uongozi unahusika na nini zaidi: malipizi, upokeaji wa sakramenti, sala, utekelezaji wa maadili na namna ya kutenda kitakatifu kazi za kila siku.

Shuhuda hizo zote na nyinginezo zinaonyesha wazi haja ya uongozi kwa jumla. Tutaelewa zaidi kwa kuzingatia hatua tatu za maisha ya Kiroho, yaani mahitaji ya wanaoanza, wanaoendelea na waliokamilika.

Uongozi wa wanaoanza

Hasa wanaoanza wanahitaji uongozi wenye busara, uimara na moyo wa kibaba, kama ule wa walezi utawani. Baadaye haja hiyo haisikiki tena vile, isipokuwa katika vipindi vigumu ambapo yanatokea mabadiliko na unatakiwa uamuzi muhimu.

Wanaoanza wanahitaji kukingwa dhidi ya marudio ya makosa na dhidi ya kasoro mbili zifuatazo zinazopingana. Baadhi wakipokea faraja za kihisi katika sala wanazidhania neema za juu, na kwa kiburi wangetaka kuruka mara hadi muungano na Mungu wasipitie hatua za lazima. Hao wanahitaji kukumbushwa haja ya unyenyekevu na kusadikishwa kuwa safari ya ukamilifu ni kazi ya maisha yote: hatuwezi kuruka bila mabawa, na katika kujenga tunaanza na misingi. Lengo ni la kwanza kutamaniwa na kukusudiwa, lakini ni la mwisho kufikiwa; tena haifai kupuuzia njia duni za lazima kulifikia. Baadhi wana kiburi cha siri katika kushika maisha magumu na kujitosa mno katika malipizi hadi kuharibu afya. Baadaye, wakitaka kujitibu wanalegea na kwenda kinyume cha awali. Hao wanahitaji kujifunza kiasi cha Kikristo na kwamba maadili ya Kimungu hayatoshi pasipo maadili ya kiutu ili kutawala polepole hisi.

Uongozi unahitajika hasa katika kipindi kirefu cha ukavu ambapo kutafakari ni kwa shida, tena kuna vishawishi vikali pamoja na upinzani wa watu. Jaribu hilo linavusha kutoka hatua ya utakaso kwenda hatua ya mwanga mradi ziwepo dalili tatu tutakazozieleza, ambazo kiongozi anatakiwa kuzitambua: 1) kutofurahia mambo ya Mungu wala ya dunia; 2) kuendelea kwa kawaida kumkumbuka Mungu, kutamani ukamilifu na kuogopa kutomtumikia; 3) kushindwa kutafakari kwa mpangilio na badala yake kuvutiwa na tendo la kumtazama tu Mungu. Katika kipindi hicho kigumu, kinachokusudiwa kuleta uongofu wa pili, ni lazima kumsikiliza kiongozi wa kufaa ili kusonga mbele kwa bidii badala ya kubaki nyuma.

Uongozi wa wanaoendelea na wa waliokamilika

Kwa kawaida uongozi wa wanaoendelea unaweza kufanyika haraka zaidi, kwa sababu wameshajua zaidi maisha ya Kiroho na mara nyingi wanaweza kueleza kwa neno moja shauri wanalohitaji linahusu nini. Hapo kiongozi ni kama shahidi wa maendeleo yao; anatakiwa kutambua kazi ya mlezi wa ndani ili awe chombo chake na kuhakikisha usikivu wao kwa Roho Mtakatifu, akipambanua ndani yao pumba na mchele, yaani kilema kikuu ambacho wapambane nacho, na mvuto maalumu wa neema ambao waufuate. Inafaa tumkimbilie kiongozi hasa wakati wa mazoezi ya Kiroho ya kila mwaka ili kumueleza kwa unyofu wote undani wa roho tusije tukajidanganya kwa kuangukia kiburi kilichofichika na kujiamini kipumbavu.

Kwa wanaoendelea pia kuna vipindi vigumu vinavyohitaji uongozi bora, hasa wanapotakiwa kuvukia hatua ya muungano. Majaribu hayo yana namna mbalimbali, lakini kwa kawaida ni kunyimwa kwa muda mrefu faraja si za hisi tu, bali za roho pia. Hapo vinatokea mara nyingi vishawishi dhidi ya imani, tumaini na upendo na unahitajika kwa namna ya pekee msaada wa kiongozi mwenye mwanga na mang’amuzi. Hata mtu anayeweza kuongoza wengine katika hatua hiyo hawezi kujiongoza kwa sababu “hakuna tena mapito tayari” (Yohane wa Msalaba), hivyo anapaswa tu kufuata mwanga wa Roho Mtakatifu asiuchanganye na msukumo mwingine unaoweza ukafanana nao.

Waliokamilika pia wanajisikia haja ya msaada huo ili kuona namna ya kulinganisha msimamo wa kujiachilia mikononi mwa Mungu na utendaji ambao Bwana anawadai, ili kutekeleza vizuri msemo huu: “kuwajibika na kujiachilia”. Wanajisikia haja ya kuongozwa ili kudumisha moyoni mwao upendo hai kwa msalaba pamoja na unyenyekevu mkubwa. Basi, ikiwa hao wanahitaji uongozi, zaidi tena wanauhitaji wanaoanza.

Sifa za kiongozi na wajibu wa anayeongozwa

Kiongozi “awe amejaa upendo, elimu na busara: likikosekana mojawapo kati ya hayo matatu, kuna hatari” (Fransisko wa Sales). “Ni muhimu sana kiongozi awe na mwanga: yaani awe na busara na mang’amuzi sana. Ikiwa zaidi ya hayo ni mwanateolojia pia, basi ni kamili. Lakini isipowezekana kuona mtu mwenye sifa hizo tatu pamoja, ni afadhali awe na zile mbili za kwanza, kwa sababu katika shida inawezekana kupata shauri la wasomi. Nionavyo mimi, hao wa mwisho, wasipojitahidi katika sala, hawafai sana kwa wanaoanza; lakini sitaki kushauri wasiwe na uhusiano nao… Elimu ni jambo kubwa… Mungu atuepushe na ibada za juujuu na zilizojaa upuuzi” (Teresa wa Yesu).

Upendo umfanye kiongozi asijitafutie faida na aongoze mioyo kwa Mungu, si kwake mwenyewe. Yohane Tauler alisema viongozi wanaojivutia watu ni kama mbwa ambao katika uwindaji wanamla mnyama badala ya kumleta kwa bwana wao; hapo huyo anawapiga kweli. Wema wa kiongozi usigeuke udhaifu: awe imara, asiogope kusema ukweli. Vilevile asipoteze muda katika maongezi na maelezo ya bure, bali alenge moja kwa moja ustawi wa roho. Awe anajua njia ya ukamilifu, mafundisho ya walimu wa Kiroho na kwa kiasi fulani saikolojia. Ili awe chombo cha Roho Mtakatifu atambue mvuto wake maalumu ambao mtu aufuate na kilema kikuu ambacho akiepe. Kwa ajili hiyo ajiombee mwanga, hasa katika kesi ngumu, na akiwa mnyenyekevu atapokea neema za kufanyia kazi yake. Ataona namna ya kusukuma wengine na kupoza umotomoto wa wengine, akiwafundisha hao wa mwisho wasichanganye mapendo ya juujuu na upendo unaothibitishwa na matendo. Busara yake katika kuongoza watu wenye bidii ikwepe hatari mbili: ile ya kutaka kufikisha wote haraka na bila tofauti kwenye sala ya hali ya juu, na ile ya kupuuzia suala hilo. Haifai kukimbia mno wala kuchelewa; kwanza zipimwe dalili tatu tulizozitaja ili kuvuka kutoka tafakuri kwenda sala ya kumiminiwa. Kabla ya kufanya hivyo, inafaa na kutosha kukumbusha watu wawe waaminifu kwa mianga ya mlezi wa ndani mara inapojitokeza kulingana na wito wao.

Wajibu wa mtu anayeongozwa unatokana na yale tuliyoyasema: amheshimu kiongozi kama wakili wa Mungu, akiepa mambo mawili, yaani kumlaumu vikali na kuhusiana naye kirafiki mno. Heshima hiyo iendane na pendo la mtoto kwa mzazi, nyofu, la Kiroho tu, linalozuia wivu wowote na hamu ya kupendwa kwa namna ya pekee. Awe na tumaini la kitoto na uwazi mkubwa kwa kiongozi wake. “Muongee naye kwa unyofu na uaminifu mkuu, mkimfunulia wazi kabisa mema yenu na mabaya yenu, bila kudanganya wala kuficha” (Fransisko wa Sales). Hatimaye, anahitaji utiifu mkubwa ili kusikiliza na kufuata mashauri yanayotolewa, la sivyo atafuata matakwa yake mwenyewe badala ya yale ya Mungu. Hakatazwi kujulisha shida kubwa iliyopo katika kutekeleza shauri fulani; lakini baada ya kufanya hivyo aweke mtazamo wake chini ya kiongozi. Hata akikosea, sisi tukimtii hatukosei, isipokuwa akitushauri kinyume cha imani au cha maadili: hapo tumuache mara.

Tusibadili kiongozi pasipo sababu nzito, hasa tukifanya hivyo kwa ugeugeu, kiburi, aibu ya kipumbavu au udadisi. Lakini tumbadili bila wasiwasi tukiona mitazamo yake ni ya kibinadamu tu, anatupenda kihisi mno, au hana elimu wala busara zinazohitajika. Nje ya nafasi hizo tudumu iwezekanavyo katika uongozi uleule ili tuzidi kufuata njia njema. Tuyakumbuke maneno ya mfalme Ludoviko IX kwa mwanae: “Uungame mara nyingi na kuchagua waungamishi wenye elimu na uadilifu ambao wajue kukufundisha la kufanya na la kukwepa, halafu uache wakuonye na kukushauri kwa uhuru wote”.

Tanbihi

Marejeo

Vyanzo bora

Maandishi ya baadaye

Viungo vya nje

Amerika Kaskazini

Ufalme wa Muungano

Australia