Mbawabuluu

Mbawa-buluu
Dume la Zizeeria knysna
Dume la Zizeeria knysna
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Lepidoptera (Nondo na Vipepeo)
Nusuoda: Glossata (Vipepeo wenye ulimi mrefu)
Familia ya juu: Papilionoidea
Familia: Lycaenidae
Nusufamilia: Polyommatinae
Swainson, 1827
Ngazi za chini

Makabila 4 :

  • Candalidini Eliot, 1973
  • Lycaenesthini Toxopeus, 1929
  • Niphandini Eliot, 1973
  • Polyommatini Swainson, 1827

Mbawabuluu ni vipepeo wadogo kiasi wa nusufamilia Polyommatinae katika familia Lycaenidae ya oda Lepidoptera. Madume wa takriban spishi zote wana mabawa ambayo upande wa juu ni buluu au urujuani kabisa au kwa sehemu. Mabawa ya majike ni kahawia au meusi na meupe. Wanatokea katika mabara yote isipokuwa Antakitiki.

Maelezo

Wapevu ni wadogo, chini ya sm 5 kwa kawaida, na mabawa yana rangi ya buluu au urujuani kwa upande wa juu, pengine na mng'ao wa metali. Mara nyingi huwa na mikia yenye nywele kama vipapasio kwenye nyuma ya mabawa ya nyuma iliyo kamili na mwonekano wa miviringo myeusi na myeupe. Spishi nyingi pia zina doa kwenye bawa la nyuma kwenye sehemu ya chini ya mkia ili kutoa mwonekano wa kichwa bandia. Baadhi yao hugeuka wanapotua ili kuwavuruga mbuai dhidi ya kutambua mwelekeo halisi wa kichwa. Hii husababisha mbuai kukaribia kutoka upande wa kichwa halisi na kusababisha ugunduzi wa mapema wa kuona au kushambulia kichwa bandia na kuishia na mdomo uliojaa kwa vigamba kama vumbi.[1]

Mara nyingi viwavi huwa bapa badala ya kuwa na umbo la mcheduara, wakiwa na tezi zinazoweza kutoa minyeso inayovutia na kuwatiisha sisimizi. Kutikulo yao huwa nene. Viwavi wa spishi fulani wanaweza kutoa mitetemo na sauti za marudio ya chini ambazo hupitishwa kupitia nyuso ambapo wanaishi. Wanatumia sauti hizi kuwasiliana na sisimizi[2][3].

Ant tending a lycaenid larva

Viwavi wa mbawabuluu ni tofauti katika tabia zao za kujilisha na mbali na kula mimea baadhi yao hula wadudu, kama vidukari, wadudu-gamba na mabuu ya sisimizi. Wengine hata hujifaidi kutoka uhusiano wao na sisimizi kwa kuwashawishi wawalishe kwa kutapika, mchakato unaoitwa trofalaksisi. Sio spishi zote zinazohitaji sisimizi, lakini angalau 80% huhusishwa na sisimizi[2], uhusiano unaoitwa myrmecophily. Uhusiano huu unaweza kuwa wa kufaidiana, wa kudusia au wa mbuai kulingana na spishi.

Kwa mfano, viwavi wa spishi fulani huhudumiwa na kulindwa na sisimizi huku wakijilisha kwa kimilewa na sisimizi hupokea mana yenye sukari kutoka kwao kwa muda wa maisha yote ya viwavi. Mabundo mara nyingi hulindwa na sisimizi pia. Katika spishi nyingine, hatua za kwanza tu hujilisha kwa kimelewa na salio la maisha ya viwavi hutumiwa ndani ya kiota cha sisimizi. Anakuwa kidusia, akila matapiko ya sisimizi, au mbuai wa mabuu ya sisimizi.[2] Viwavi huwa mabundo ndani ya kiota cha sisimizi na hao huendelea kuwachunga mabundo. Muda mfupi kabla ya wapevu kuibuka mabawa ya kipepeo ndani ya kifuko cha bundo hujitenga nayo na bundo anapata rangi ya fedha. Kipepeo aliyekomaa hutoka kwa bundo baada ya wiki tatu hadi nne, akiwa bado ndani ya kiota cha sisimizi. Lazima kipepeo atambae kutoka kwenye kiota kabla ya kupanua mabawa yake.

Mageuko kadhaa ya kutohoa huwezesha uhusiano huu, ikiwa ni pamoja na tezi ndogo kwenye ngozi ya viwavi inayoitwa "pore cupola organs". Pia wana tezi kwenye pingili ya saba ya fumbatio inayotoa mana na inaitwa "tezi ya mana ya mgongo". Jozi ya viungo vinavyoweza kuchomoza viitwavyo "viungo vifananavyo vipapasio" vipo kwenye pingili ya nane ya fumbatio. Viungo hivyo vina umbo la mcheduara na vina mviringo wa miiba juu yao. Vinatoa ishara za kemikali ambazo zinaaminika kusaidia katika mawasiliano na sisimizi.[4]

Mfano wa uhusiano kati ya kipepeo na sisimizi katika Afrika ya Mashariki ni ule kati ya Anthene usamba na sisimizi wa Crematogaster mimosae[5]. Hawa huishi kwenye miti ya mbalibali (Vachellia drepanolobium) ambayo huwatolea sisimizi makazi katika vitako vya miiba vilivyovimba na vinavyoitwa domatio. Majike wa A. usamba wanapendelea kutaga mayai kwenye majani na matawi machanga ya mbalibali. Baada ya muda mfupi wa kujilisha kwa majani machanga, viwavi huingia domatio zilizo karibu, kiwavi mmoja katika domatio moja. Hapa, hulishwa na sisimizi au hujilisha kwa mabuu ya sisimizi (bado haijagunduliwa). Wanakuwa bundo katika domatio pia na wapevu wanaoibuka huondoka kupitia shimo lililotafunwa na kiwavi.

Spishi kadhaa za Afrika ya Mashariki

  • Actizera lucida
  • Anthene ligures
  • Anthene usamba
  • Azanus ubaldus
  • Cacyreus lingeus
  • Chilades kedonga
  • Cupidopsis iobates
  • Eicochrysops hippocrates
  • Eicochrysops masai
  • Euchrysops malathana
  • Euchrysops subpallida
  • Freyeria trochylus
  • Harpendyreus aequatorialis
  • Lampides boeticus
  • Lepidochrysops kitale
  • Leptotes adamsoni
  • Leptotes pirithous
  • Neurellipes gemmifera
  • Phlyaria cyara
  • Pseudonacaduba sichela
  • Tarucus grammicus
  • Thermoniphas micylus
  • Triclema nigeriae
  • Tuxentius calice
  • Tuxentius cretosus
  • Uranothauma nubifer
  • Zintha hintza
  • Zizeeria knysna
  • Zizina antanossa
  • Zizula hylax

Picha

Marejeo

  1. Robbins, Robert K. (1981). "The 'False Head' Hypothesis: Predation and Wing Pattern Variation of Lycaenid Butterflies". American Naturalist. 118 (5): 770-775.
  2. 2.0 2.1 2.2 Pierce, N. E.; Braby, M. F.; Heath, A.; Lohman, D. J.; Mathew, J.; Rand, D. B. & Travassos, M. A. (2002). "The ecology and evolution of ant association in the Lycaenidae (Lepidoptera)". Annual Review of Entomology. 47: 733-771.
  3. DeVries, Philip J. (1992). "Singing Caterpillars, Ants and Symbiosis". Scientific American, 267: 76
  4. "Lycaenid Butterflies and Ants". Australian Museum. Archived 18 November 2007.
  5. Martins, D.J. et al. (2013) Ushirikiano kati ya lycaenid ya Kiafrika, Anthene usamba, na chungu wa acacia obligate, Crematogaster mimosae. Jarida la Biolojia 109: 302-312.