Misimu (lugha)

Misimu (pia simo; Kiing. jargon, patois, cant, slang) ni maneno yasiyo sanifu yanayoanzishwa na kikundi cha watu fulani wenye utamaduni mmoja ili kueleza mahusiano yao kama kikundi. Mara nyingi maneno hayo huzuka na kupotea, ila yale yanayodumu yanaweza kusanifiwa na kuwa msamiati rasmi wa lugha.

Maana

Tovuti ya Swahilihub inaeleza: "Misimu ni jumla ya maneno yote ambayo siyo sanifu katika lugha yoyote mathalani Kiswahili ambayo yameibuliwa na vikundi vidogo vya watu wenye utamaduni unaofanana kwa lengo la kuwa na usemi mmoja unaolinda, mawazo na mawasiliano vya wanavikundi. Sababu ya kuitwa misimu ni kuwa maneno hayo huzuka na kupotea na mara nyingi kulingana na matukio fulani katika jamii husika."

Chanzo

Mabadiliko ya kihistoria yanaoikumba jamii katika shughuli mbalimbali na miongoni mwa utu wa watu mbalimbali.

Kwanza ni matukio mbalimbali yanayojitokeza katika jamii; matukio hayo yanaweza kuwa vita, njaa, ukame na kadhalika. Misimu hiyo yaweza kuwa ni ya kubeza, kusifu na kukejeli.

Ya pili ni uwepo wa matabaka, uwepo wa tofauti za kimaisha katika jamii fulani: kwa mfano, walalahoi ni maskini na magambacholi ni wenye nazo.

Ya tatu ni utani, utamaduni wa kutaniana. Jambo lingine linalosababisha kuzuka kwa misimu, msimu huu hubeba kejeli na dhihaka.

Ya nne ni maendeleo ya sayansi na teknolojia: hayo pia huwa chanzo cha misimu; vitu vipya vinavyojitokeza katika jamii vinadai uwepo wa maneno yanayozuka, kwa mfano, bajaji na digitali.

Sifa

  1. Huzuka na kutoweka kufuatana na mabadiliko ya jamii
  2. Ni lugha isiyosanifiwa
  3. Ni lugha ya mafumbo
  4. Hupendwa na watu wengi kwa sababu hufurahisha
  5. Ni lugha inayofahamika na watu wachache
  6. Huwa na chumvi nyingi.

Aina za misimu

Katika misimu kuna aina tatu ambazo ni:

  1. Misimu ya pekee: misimu hii huelezea uhusiano wa kikundi kidogo kwenye utamaduni mmoja ambayo huweza kuwa shule moja, mtaa mmoja, ofisi moja na kadhalika.
  2. Misimu ya kitarafa: misimu hii huchukua eneo pana kidogo, kwa mfano kata, wilaya na hata mkoa.
  3. Misimu zagao: misimu hii huenea karibu nchi nzima; wakati mwingine huvuka nchi: kwa mfano, Wapemba na wakereketwa.

Dhima au kazi

Sababu ya kutumia misimu ni:

  1. kuunganisha watu tofauti ili kutunza historia ya jamii fulani
  2. kukuza lugha
  3. kupamba lugha
  4. kufanya mawasiliano yawe mafupi
  5. kuibua na kubaini hisia mbalimbali za wazungumzaji
  6. kufurahisha na kuchekesha kwa kuwa haina chuki wala kejeli
  7. kuficha lugha ya matusi kwa kupunguza ukali wa maneno (kwa mfano: kula raha = kufanya ngono)
  8. kukosoa na kuiasa jamii (kwa mfano: fataki).
  9. kutumika kama kitambulisho cha kundi fulani la watu

Njia za kuunda msimu

  1. Kufupisha maneno (kwa mfano: kk, yaani kula na kulala)
  2. Kutohoa maneno ya lugha za kigeni
  3. Kutumia silabi ni utenganisho wa umbo, rangi, kiini, dhima baina ya watu
  4. Kutumia sitiari/jazanda.
  5. kutumia tanakali sauti nyingine.
  6. Kugeuza mpangilio wa maneno.

Sababu za kutumia msimu

  1. Kuhitaji mazungumzo ya siri ili wasiohusika wasielewe
  2. Kudhani ndio ujuzi wa lugha
  3. Kuongeza uzuri na ukali wa jambo wakati wa kulikamata n.k.

Matatizo ya misimu

Matatizo yanayojitokeza katika misimu ni kwamba:

  1. huharibu lugha sanifu,
  2. mara nyingi huleta msamiati wenye matusi,
  3. hupunguza hadhira,
  4. huzuka na kutoweka,
  5. ni lugha ya mafumbo,
  6. ina maana nyingi.
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Misimu (lugha) kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.