Mlangobahari wa Palk

Mlangobahari wa Palk, Daraja la Adamu, Ghuba ya Bengali.
Daraja la Adamu.

Mlangobahari wa Palk (kwa Kiingereza: Palk Strait) ni sehemu ya bahari baina ya Uhindi na Sri Lanka. Upana wake ni kilomita 53 hadi 82. Unaunganisha Ghuba ya Bengali kwenye kaskazini na Ghuba ya Mannar iliyoko upande wa kusini. [1]

Jina la mlangobahari huo linatunza kumbukumbu ya Mwingereza Robert Palk aliyekuwa gavana wa jimbo la Madras (1755-1763) wakati wa utawala wa Kampuni ya Kiingereza kwa Uhindi ya Mashariki.

Kusini mwa mlangobahari huo kuna safu ya visiwa vidogo na miamba tumbawe inayopita kutoka Uhindi hadi Sri Lanka. Visiwa hivyo huitwa "Daraja la Rama" na Wahindu au "Daraja la Adamu" na Waislamu na pia kimataifa (Adam's Bridge)[2].

Kuanzia mwaka 1914 kulikuwa na njia ya reli kutoka Madras hadi Dhanushkodi, kutoka hapo feri ilibeba mabehewa hadi kisiwa cha Mannar na kutoka hapo njia ya reli ikaendelea hadi Colombo. Tangu dhoruba kali ya mwaka 1964 kituo cha Dhanushkodi kiliharibiwa na ratiba haijarudishwa bado. Mwaka 2011 marais wa Uhindi na Sri Lanka walipatana kurudisha angalau huduma ya feri[3].

Visiwa na miamba tumbawe kwenye Daraja la Adamu vinazuia usafiri wa meli kubwa zinazopaswa kuzunguka Sri Lanka yote. Tangu siku za ukoloni kulikuwa na mipango ya kuchimba mfereji wa meli unaokata daraja la Adamu. Mwaka 2004 serikali ya Tamil Nadu ilifanya utafiti kuhusu gharama na athira ya kuchimba njia ya meli hapo. Mpango huu ulipingwa na wafuasi wengine wa imani ya Uhindu; katika msahafu wao wa Ramayana kuna simulizi kwamba mungu Rama alijenga daraja hadi Sri Lanka kwa msaada wa mfuasi wake Hanuman katika vita ya kupambana na jeshi la pepo. Wapinzani hao huamini kwamba Daraja la Adamu ni sawa na daraja lililojengwa na Rama. Wataalamu wengine Wahindi walipinga maelezo hayo wakidai eti, daraja la Rama ni tofauti na safu ile ya visiwa[4].

Tangu mwaka 2016 kuna mpango wa kujenga handaki chini ya bahari litakalorahisiha mawasiliano na kustawisha uchumi kati ya nchi mbili[5].

Marejeo

  1. Map of Sri Lanka with Palk Strait and Palk Bay
  2. "Adam's bridge". Encyclopædia Britannica. 2007. Iliwekwa mnamo 2007-09-14.
  3. Sri Lanka, India to relaunch ferry service after three decades, tovuti ya Pakistan Today ya 7 Januari 2011, iliangaliwa Oktoba 2019
  4. Hanuman bridge is myth:Experts, tovuti ya Times of India, tar. 18 Oktoba 2002, iliangaliwa Oktoba 2019
  5. The Tunnel from India to Sri Lanka Ilihifadhiwa 3 Januari 2020 kwenye Wayback Machine., tovuti ya Indianrailways.gov ya arehe 6 Januari 2016, iliangaliwa Oktoba 2019

Viungo vya Nje

Wikimedia Commons ina media kuhusu:

10°00′N 79°45′E / 10.000°N 79.750°E / 10.000; 79.750