Seti I

Picha ya Sethi kwenye hekalu aliyojenga pale Abydos
Hieroglyphs kutoka kaburi la Seti I

Seti I (au Sethos I kwa Kigiriki) alikuwa farao wa nasaba ya 19. Kipindi chake huhesabiwa katIka Ufalme Mpya. Alikuwa mtoto wa Ramses I na Malkia Sitre, na baba wa Ramses II.

Kama ilivyo na tarehe zote katika Misri ya Kale, tarehe halisi za utawala wake hazijulikani. Wanahistoria anuwai wanataja tarehe tofautitofauti, na 1294 KK hadi 1279 KK [1]. 1290 KK hadi 1279 KK [2] ni tarehe zinazokubaliwa zaidi na wasomi wa leo.

Jina 'Seti' linadokeza kwamba alilipokea kwa heshima ya mungu Set (au "Seth"). Kama ilivyo kwa mafarao wengi, Seti alikuwa na majina kadhaa. Wakati wa kupokea ufalme alichukua jina la binafsi "mn-m3'tr' ", ambalo kwa kawaida hutamkwa Menmaatre. Katika lugha ya Kimisri maana yake ni "Milele ni Haki ya Re". Jina linalojulikana zaidi alilopata wakati wa kuzaliwa ni "sty mry-n-pth" au Sety Merenptah, maana yake "Mtu wa Set, mpendwa wa Ptah".

Mafanikio makubwa zaidi ya sera za kigeni za Seti I yalikuwa kuteka mji wa Kadesh katika Syria pamoja na eneo jirani la Amurru lililowahi kutawaliwa na Milki ya Wahiti.

Seti alifaulu kushinda jeshi la Wahiti ambalo lilijaribu kulinda mji. Aliingia mjini kwa shangwe pamoja na mwana wake na mrithi Ramses II akaweka jiwe la ushindi. Kadesh, hata hivyo, baada ya muda ilirudi chini ya udhibiti wa Wahiti kwa sababu Wamisri hawakuweza kudumisha ulinzi wa kudumu kule Kadesh na Amurru.

Seti I ametuachia jiwe la kumbukumbu ya vita zake ambalo hutukuza mafanikio yake, pamoja na maandiko kadhaa, ambayo yote huwa yanakuza mafanikio yake ya binafsi kwenye uwanja wa vita. [3]

Marejeo

  1. Michael Rice (1999). Who's Who in Ancient Egypt. Routledge.
  2. J. von Beckerath (1997). Chronologie des Äegyptischen Pharaonischen (kwa German). Phillip von Zabern. uk. 190.{cite book}: CS1 maint: unrecognized language (link)
  3. Brand, Peter J. 2000. The Monuments of Set I: epigraphic, historical and art historical analysis. Brill.