Kiarabu
Kiarabu (ar.: العَرَبِيَّة, al-ʻarabiyyah, kwa kirefu al-luġatu al-ʿarabiyya) ni lugha ya Kisemiti inayotumiwa na watu milioni 206 kama lugha ya kwanza[1] na milioni 246 wa ziada kama lugha ya pili. Ilhali kuna lahaja nyingi, Kiarabu sanifu (ar. الفصحى fuṣḥā) ni lugha rasmi ya nchi 22 za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya Mkutano wa Kilele wa Kiislamu na mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa. Kuna pia matumizi kama lugha ya kidini katika Uislamu.
Hivyo Kiarabu ni mojawapo ya lugha muhimu sana duniani ikisomwa kwa viwango tofauti na mamilioni ya waumini Waislamu wakielekea kujifunza na kuelewa kitabu cha Korani. Kama lugha ya kidini ina athari na taathira kubwa juu ya lugha nyingi ulimwenguni na juu ya ustaarabu na utamaduni wa watu na makabila tofautitofauti walio Waislamu.
Kiarabu kwa kawaida huandikwa kwa herufi za Kiarabu.
Ni lugha yenye utajiri mkubwa wa misamiati (maneno), ufasaha mkubwa wa misemo na udhibiti mkubwa wa sarufi na nahau.
Ni lugha iliyokusanya aina nyingi za mithali na mafumbo, na ina utamaduni mkubwa wa nyimbo, mashairi na misemo, nayo inakubaliwa na watu wengi duniani kuwa lugha yenye utamu wa matamshi na uzuri wa lafudhi.
Kwa kuwa Qurani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad na Mashairi ya zama za Ujahili ndio yenye kudhibiti lugha hii isitetereke wala kubadilika na kupotea kama lugha nyingine nyingi, leo, baada ya miaka zaidi ya elfu, imebaki thabiti kama ilivyokuwa wakati ilipoandikwa Qurani, na mabadiliko yoyote yaliyotokea hayana uhusiano na lugha yenyewe ya Kiarabu, bali yana uhusiano na lahaja na vilugha mbalimbali zinazotumika na Waarabu wa sehemu fulani ya nchi au mji. Ama lugha rasmi ya Kiarabu basi imedhibitika kulingana na Qurani na Sunnah, ili maandishi hayo yaendelee kufahamika milele.
Leo, Kiarabu ni lugha ya sita ulimwenguni kwa wingi wa wanayoitumia kila siku katika maisha yao, baada ya Kichina, Kihindi, Kihispania, Kiingereza na Kibengali.
Umuhimu wa lugha hii unazidi kukua kila siku kwa sababu ya kutumika kwenye maeneo ya katikati ya ulimwengu baina ya mabara ya kale (Afrika, Asia na Ulaya) na mabara mapya ya ulimwengu (Amerika ya Kaskazini na Kusini).
Asili ya lugha ya Kiarabu
Kiarabu, pamoja na lugha ya Kiebrania (ya Uyahudi) na Kiaramu (ya Mashariki ya Kati) na Kiamhari (ya Ethiopia) zinatokana na asili moja ya lugha ya Kisemiti. Kuna lugha nyingi vile vile ambazo zinatokana na asili hii, kama Kiashuri, Kifinisia, Kibabili na kadhalika. Baadhi ya hizi lugha zimekufa au kuwa na wazungumzaji wachache, na kwa hiyo umuhimu wake umekuwa si mkubwa kama ulivyo umuhimu wa lugha ya Kiarabu.
Aina za Kiarabu
Kuna aina tatu kubwa za lugha hii ya Kiarabu:
- Kiarabu Fasihi ambacho kilikuwa kikitumika zama za Ujahili kabla ya kuja Uislamu, na kuendelea kutumika baada ya kuja Uislamu katika Qurani na Sunnah za Mtume Muhammad,
- Kiarabu Mamboleo ambacho kinatumika katika maandishi na mazungumzo rasmi baina ya Waarabu wote kwa jumla, na
- Kiarabu Lahaja ambacho kinatumika na watu maalumu katika sehemu fulani za nchi au vijiji, na ni lugha ya mahali tu, kama vile Kiyemeni au Kimasri au Kishami au Kimaghribi, na lugha hizi au lahaja hizi zinakuwa zinatofautiana sana baina yake katika misamiati na matumizi.
Kiarabu fasihi
Kiarabu ni lugha ya zamani sana (tarehe yake inarudi nyuma zaidi ya miaka 2000), nayo pamoja na lugha nyinginezo za Kisemiti zilikuwa zikitumika katika nchi za Mashariki ya Kati. Kiarabu Fasihi ilianza kuwa na nguvu zaidi baada ya kuteremshwa Qurani kwa lugha hiyo na kuhifadhiwa Hadithi za Mtume Muhammad na kuwa ndio chanzo cha lugha zote nyinginezo za Kiarabu zilizokuweko wakati huo.
Fasihi ya Kiarabu isiyo na tabia ya kidini ilikuwa hasa Ushairi. Washairi kama Abu Nuwas, Omar Khayyam, Hafiz, ibn Qayyim al-Jawziyyah wanakumbukwa hadi leo. Masimulizi kama Alfu Lela U Lela hayakuwa fasihi yenyewe, hata kama yamepata umaarufu katika nchi za Ulaya.
Maandishi mengine ya Kiarabu yaliyokuwa muhimu sana ni maandiko ya falsafa na sayansi. Waarabu walitafsiri maandiko ya Wagiriki wa Kale wakaendeleza ujuzi wao. Katika karne zilizopita Ulaya ilipokea sehemu kubwa ya elimu yake kutoka kwa Waarabu kwa njia hiyo.
Tangu karne ya 19 na katika karne ya 20 fasihi ya Kiarabu imepata uamsho mkuu. Khalil Jibran wa Lebanon yuko kati ya washairi wanaosomwa zaidi kimataifa. Nagib Mahfuz wa Misri ni mwandishi Mwarabu wa kwanza aliyepokea Tuzo ya Nobel ya Fasihi mwaka 1988.
Tanbihi
- ↑ https://www.ethnologue.com/language/arb Arabic, Standard kwenye tovuti ya ethnologue