Saint Helena

Bendera ya St. Helena
Bendera ya St. Helena
Lugha rasmi Kiingereza
Mji Mkuu Jamestown
Serikali Eneo la ng'ambo la Uingereza
Mkuu wa Dola Elisabeth II
Gavana Michael Clancy
Eneo (pamoja na visiwa vya pembeni) 414 km²
Idadi ya Wakazi 4,897 (Juni 2018)
Wakazi/km² 35
Pesa Pauni ya St. Helena
Saa za eneo UTC
Wimbo la Taifa God Save the Queen
St. Helena na visiwa vya jirani katika Atlantiki
Mahali pa St. Helena mbele ya Afrika)

Saint Helena (maana kwa Kiingereza: Mtakatifu Helena) ni kisiwa cha bahari ya Atlantiki ya kusini chenye eneo la km² 122.

Umbali na Angola ni km 1.868, ni km 3.290 hadi Brazil (Amerika ya Kusini).

Kisiwa, chenye asili ya kivolkeno, kimo ndani ya beseni la Angola la Atlantiki, hivyo huhesabiwa kuwa kisiwa cha Afrika.

Kiutawala ni eneo la ng'ambo la Uingereza na makao makuu ya kundi la visiwa vidogo pamoja na kisiwa cha Ascension na funguvisiwa la Tristan da Cunha.

Mji mkuu ni Jamestown, wenye wakazi 900.

Historia ya Wakazi

Wakazi 4,897 (2018) ni wa asili ya Ulaya, Afrika na China. Wote wana uraia wa Uingereza wakitumia lugha ya Kiingereza.

Kihistoria Saint Helena haikuwahi kuwa na wakazi kabla ya kufika kwa Wareno mwaka 1502 BK: ndio waliojenga nyumba za kwanza bila kuacha wakazi wa kudumu.

Katika miaka iliyofuata palikuwa na mvutano kati ya Wareno, Waholanzi na Waingereza.

Tangu mwaka 1673 Kampuni ya Kiingereza ya India ya Mashariki ilitawala kisiwa kama kituo cha safari za merikebu ya matanga kubwa kati ya Uingereza, Afrika ya Kusini na India. Kampuni ilianzisha mji wa Jamestown na mashamba makubwa ya mboga kwa ajili ya mabaharia waliopita huko. Kwa ajili hiyo watumwa Waafrika walipelekwa Saint Helena; baada ya mwisho wa utumwa katika karne ya 19 pia wafanyakazi Wahindi, Wamadagaska na Wachina.

Longwood House, St Helena: nyumba alimoishi Napoleon wakati wa kufungwa kisiwani

Napoleon

Jina la Saint Helena lilipata kujulikana kote duniani kutokana na kuwa mahali pa kufungwa kwa Kaisari Napoleon I. wa Ufaransa. Napoleon alikuwa kiongozi aliyeogopwa sana na kutawala sehemu kubwa ya Ulaya kwa miaka kadhaa mwanzoni wa karne ya 19.

Baada ya kushindwa mwaka 1814 huko Lipsia alitakiwa kubaki kwenye kisiwa cha Elba (Italia), lakini alitoroka na kuanza vita upya.

Baada ya kushindwa mara ya pili huko Waterloo, Waingereza walimpeleka mahali pa mbali iwezekanavyo, St. Helena, mwaka 1815. Hapo aliishi katika hali ya kufungwa akiwa na nyumba yake na watumishi wake, lakini alipaswa kuongozana kisiwani na maafisa Waingereza waliomfuata kila alikokwenda. Kwa ujumla Waingereza walipeleka St. Helena wanajeshi 2,000 pamoja na mabaharia wa kijeshi 500 ili wamlinde Napoleon wakiogopa majaribio ya Wafaransa kumwondoa na kumrudisha katika hali ya uhuru.

Napoleon alikufa mwaka 1821 akazikwa kisiwani, lakini mwili wake ulihamishwa baadaye kwenda Ufaransa alikopewa kaburi la heshima Paris mjini.

Ufaransa ilinunua baadaye nyumba alimoishi kutoka kwa Uingereza kama makumbusho ya kitaifa pa Ufaransa hadi leo.

Hali ya St. Helena leo

Kisiwa kinafikiwa kwa meli tu, haina kiwanja cha ndege kikubwa. Lakini hakuna meli za tanga tena zinazohitaji kusimama St. Helena na kuchukua maji pamoja na chakula. Hivyo hali ya uchumi ni duni.

Kuna uvuvi kidogo na utalii unaotegemea kumbukumbu ya Napoleon. Kuna meli moja tu ya kuhudumia St. Helena na visiwa vingine: inafika takriban mara mbili kwa mwezi. Muda wa safari kati ya St. Helena na Namibia au Afrika Kusini ni siku 4 au 5.

Kwa ujumla kisiwa kinategemea misaada ya serikali ya Uingereza.


Nchi za Afrika Bara la Afrika
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira