Shetani

Shetani kadiri ya William Blake
Anguko la Shetani kadiri ya Gustave Doré

Shetani (kwa Kiebrania שָׂטָן Satan, kwa Kigiriki Σατανᾶς Satanâs, kwa Kilatini Sátanas) ni jina linalomaanisha "Mpinzani"; "Mshtaki".

Shetani anajulikana pia kama Ibilisi (kutoka Kigiriki Diabolos, -ou, "Anayetenganisha"), Mtawala wa giza, Mkuu wa ulimwengu huu, Belzebub (jina la dhihaka kwa mungu Baal linalotafsiriwa "Bwana wa nzi"), Belial, Lusiferi (kutoka Kilatini Lucifer, "Mleta mwanga").

Kadiri ya imani ya dini mbalimbali, hasa zile zinazokubali ufunuo waliopewa Waisraeli, shetani ni malaika, roho, au mungu mdogo anayewakilisha uovu unaopingana na Mungu. Baadhi ya watu, kwa mfano Wakristadelfiani, hufundisha kwamba Shetani si nafsi hai, bali mfano tu wa uovu na dhambi.

Utendaji wake

Dhuluma za shetani ni zile zote tunazoweza kuteswa naye, yaani:

  1. kushawishiwa,
  2. kupatwa na
  3. kupagawa.

Kuhusu hayo neno la teolojia ya Kikristo linaloyaangaza yote ni kwamba kazi ya shetani haivuki kamwe hisi zetu isiweze kutendeka moja kwa moja katika akili na utashi. “Mungu tu aliweza kuelekeza akili yetu kwenye ukweli wote na utashi wetu kwenye wema wote, na hatimaye kama lengo kuu kwake mwenyewe aliye wema mkuu. Kwa hiyo yeye tu anaweza kutenda moja kwa moja katika akili yetu na utashi wetu, kadiri ya elekeo la umbile ambalo mwenyewe aliliweka na analidumisha ndani ya vipawa hivyo” (Thoma wa Akwino). Mungu tu anapenya roho. Kwa ruhusa yake shetani anaweza akatushambulia akitenda katika ubunifu wetu, hisi zetu, vitu vya nje na mwili wetu ili kututia maovuni.

Tujihadhari tusizidhishe pande mbili tofauti: ama kumhusisha shetani na yale yanayotokana na tabia mbovu (kiburi na tamaa) au na maradhi; ama kutokubali kamwe uwepo wa athari yake wala kujali yale yanayofundishwa na Maandiko na Mapokeo matakatifu kwa Wakristo au na misahafu kwa Waislamu.

Kushawishwa

Watu wanapatwa na vishawishi kwa sababu mbalimbali, kama vile ubovu wa moyo na mazingira, lakini ikiwa ni vya ghafla, vya nguvu na vya kudumu na havielezeki kwa maradhi yoyote, inawezekana kuviona vimeathiriwa na shetani kwa namna ya pekee.

Kupatwa

Yeye anaweza akatenda: katika uwezo wa kuona kwa maono ya kuchukiza au ya kupendeza; katika uwezo wa kusikia kwa kusababisha kelele au kufanya yasikike maneno ya kufuru au ya uzinifu; katika uwezo wa kugusa kwa kupiga au kwa kupapasa kimapenzi. Pengine hayo hayatokei mwilini bali katika ubunifu au yanatokana na mhemko wa mishipa ya neva.

Kazi ya moja kwa moja ya shetani katika ubunifu, kumbukumbu na maono inaweza ikasababisha taswira zisizobanduka ingawa mtu anafanya juu chini azifukuze na ambazo zinaleta hasira, chuki, pendo la hatari au fadhaiko la kukatisha tamaa. Pengine wanaodhulumiwa hivyo wanahisi kwamba ubunifu wao ni kama umefungwa na giza nene na kwamba moyo wao unalemewa na uzito unaowakandamiza. Ni utovu wa nguvu ulio tofauti na ule unaotokana na kazi ya Mungu ambaye akijalia kuzama katika mafumbo anasababisha tafakuri karibu isiwezekane. Adui yake, akitamani kwa wivu kumuiga, anajitahidi kuchepusha matokeo ya kazi hiyo, hivi kwamba katika matakaso ya Kimungu mtu anajikuta pengine kati ya utendaji wa Mungu, unaomuelekeza maisha ya Kiroho yasiyotegemea zaidi hisi, na utendaji wa adui unaomsababishia kwa namna yake utovu wa nguvu ili kumchanganya.

Maria wa Yesu Msulubiwa alipatwa na majaribu ambayo ni kati ya yale makubwa zaidi yanayoweza yakaendana na matakaso ya Kimungu na ambayo yanadhihirisha ukweli wa maneno ya Yohane wa Msalaba: “Ni vita vya wazi kati ya roho mbili… Mungu kadiri na jinsi anavyomvuta mtu anamruhusu shetani atende dhidi yake kwa namna hiyo… Pengine shetani anamtisha sana mtu: duniani hakuna teso la kufanana na hilo. Roho inaishirikisha roho hofu yake”.

Kupagawa

Katika kupagawa shetani anakaa mwilini mwa mhusika, badala ya kutokeza tu utendaji wake toka nje inavyotukia katika kupatwa naye. Akitenda hivyo toka ndani, hazuii tu utendaji wa hiari wa vipawa vya mtu, bali anasema na kutenda mwenyewe kupitia viungo vya mtu, bila huyo kuweza kumzuia na kwa kawaida hata kutambua. Shetani hamkalii mtu kama roho inavyohuisha mwili wake, bali kama mota ambayo kupitia mwili inatenda rohoni. Anatenda moja kwa moja katika viungo vya mwili vifanye matendo ya kila aina, na kwa njia yake anatenda katika vipawa kadiri vinavyotegemea mwili kwa kutenda kazi.

Wakati wa upeo wa hali hiyo kwa kawaida mhusika anapotewa na hisi yoyote ya mambo yanayomtokea, kwa sababu baadaye hakumbuki lolote isipokuwa mara mojamoja. Wakati wa utulivu ni kana kwamba shetani amejiondokea, ingawa pengine yanabaki maradhi ya kudumu ambayo madaktari wanashindwa kuyatibu.

Kwa kawaida kupagawa ni adhabu kuliko jaribu la kutakasa, lakini katika watu waliojitoa mhanga kwa ajili ya wakosefu hali hiyo inaweza ikaendana na takaso la Kimungu la hisi au la roho.

Dalili za kupagawa kweli

Ni kusema kwa lugha isiyojulikana au kumuelewa mtu anayeiongea; kuvumbua mambo ya mbali na ya siri; kuonyesha nguvu inayozidi ile ya kimaumbile ya mhusika, kulingana na umri na hali yake. Dalili hizo na nyinginezo, hasa zikipatikana nyingi kwa pamoja, zinatufanya tushuku mtu amepagawa. Kwa namna ya pekee zinashtusha ikiwa k.mf. mtu asiyejua Kilatini wala teolojia anakuja kusema Kilatini kwa ufasaha kuhusu masuala magumu ya teolojia.

Dalili nyingine ya kupagawa ni mtu kukasirika na kumkufuru Mungu kwa namna ya kutisha akiguswa kwa kitu kitakatifu au akiombewa kwa sala fulani. Dalili hiyo ni wazi zaidi ikiwa anaguswa au kuombewa bila yeye kujua, hivi kwamba itikio hilo lisiweze kutokana na hiari yake kwa ubaya au kwa kujifanya amepagawa.

Katika umanyeto wa hali ya juu yanatokea mambo ya namna hiyo, ingawa si kiasi cha kumfanya mgonjwa atoe hoja kwa lugha asiyoijua au juu ya suala asilolielewa. Tena shetani anaweza akasababisha maradhi ya akili au matukio ya nje yanayofanana nayo; anaweza vilevile kutumia maradhi yaliyopo na kumkatisha mgonjwa tamaa.

Dawa za kupagawa kadiri ya Kanisa Katoliki

  1. Kufanya toba na kutakasa dhamiri kwa kuungama vema.
  2. Kupokea ekaristi mara nyingi kufuatana na shauri la padri mwenye busara na mwanga. Kadiri tulivyo safi na wenye toba shetani hana uwezo juu yetu, na ekaristi takatifu inatupatia Yesu, yule ambaye alitustahilia neema na kumshinda shetani. Hata hivyo komunyo iruhusiwe tu wakati wa utulivu.
  3. Kuomba mara nyingi huruma ya Mungu kwa sala na mfungo.
  4. Kukimbilia kwa tumaini jina takatifu la Yesu na kutumia kwa imani kubwa visakramenti, hasa ishara ya msalaba na maji ya baraka.
  5. Hatimaye kwa ukombozi wa waliopagawa yamewekwa mazinguo kutokana na mamlaka ya kufukuza mashetani ambayo Yesu Kristo ameliachia Kanisa. Lakini mazinguo makuu yanaweza kufanywa na mapadri wale tu walioteuliwa na kupewa ruhusa maalumu na askofu wa jimbo.

Marejeo