Siku ya pai

Keki ya pai iliyoandaliwa kwenye chuo kikuu cha Delft (Uholanzi)
Larry Shaw mwanzilishaji wa sikukuu ya pai pamoja na keki za sherehe

Siku ya pai au siku ya π ni sikukuu ya kusheherekea namba π. Husheherekewa na wanahisabati na marafiki wa hisabati duniani. Pai inayoitwa pia "namba ya duara" ni namba isiyowiana ilhali thamani yake hukaribia 3.14159265358.. au chamkano cha 22/7 lakini haiwezi kutajwa kikamilifu kwa njia hizi.

Tarehe mbili

Kutokana na thamani hizi kuna siku mbili zinazosheherekewa ambayo ni 14 Machi (kwa namna ya Kimarekani tarehe hii huandikwa 3-14) na pia 22 Julai inayoweza kuandikwa kwa namna ya kufanana na chamkano 22/7. Kwa Kiingereza 14 Machi huitwa "Pi-Day" na 22 Julai "Pi Approximation Day". Hali halisi 22/7 iko karibu zaidi na thamani halisi ya π kuliko 3.14.

14 Machi huangaliwa zaidi katika nchi zinazoandika tarehe zao kwa namna ya mwezi-siku kama Marekani, na 22 Julai hupendelewa katika nchi zinazoandika tarehe kwa namna ya siku-mwezi.

Chanzo cha sikukuu

Sherehe ya sikukuu ya pai ilianzishwa na mwanafizikia Larry Shaw kama mbinu wa kuvuta wageni katika makumbusho ya kisayansi unaoitwa exploratorium mjini San Francisco (Marekani). Walitaka kuonyesha hisabati na sayansi kwa njia y kuvutia kwa hiyo walianzisha sherehe katika chumba kipya chenye umbo la duara. Wakasheherekea kwa kuandaa na kula keki za mviringo (zinazoitwa "pie" kwa Kiingereza, neno la kufanana na matamshi ya Kiingereza ya "pi").

Polepole sherehe ilianza kusambaa hasa baada ya kupokelewa na walimu wa hisabati kama nafasi nzuri ya kuonyesha hisabati pamoja na mizaha kadhaa na kula keki za mviringo wakati wa vipindi. Harakati ya kusambaza sikukuu hiyo iliongezeka baada ya kutambua ya kwamba tar. 14 Machi ni pia sikukuu ya kuzaliwa kwa Albert Einstein.

Siku ya pai kwenye 22 Julai humkumbuka hasa mtaalamu wa kale Archimedes aliyetambua thamani ya pai kukarbia 22/7.

Viungo vya Nje