Fupefupe

Fupefupe
Fupefupe (Chanos chanos)
Fupefupe (Chanos chanos)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Nusufaila: Vertebrata (Wanyama wenye uti wa mgongo)
Ngeli: Actinopterygii
Oda: Gonorynchiformes
Familia: Chanidae
Günther, 1868
Jenasi: Chanos
Lacépède, 1803
Spishi: C. chanos
(Forsskål, 1775)

Fupefupe, borodi au mwatiko ni spishi ya samaki ya baharini (Chanos chanos) katika familia Chanidae. Jina mwatiko hutumika kwa spishi za dagaa pia.

Maelezo

Fupefupe wanaweza kukua hadi m 1.80 lakini mara nyingi hawana urefu wa zaidi ya m 1. Wanaweza kufikia uzito wa kg 14 na umri wa miaka 15. Wana mwili uliorefuka ambao umefinywa na kuwa na umbo linganifu na laini, pezimgongo moja, mapeziubavu yenye umbo la mabawa ya kozi na pezimkia kubwa kiasi wenye panda. Kinywa ni kidogo na hakina meno. Rangi ya mwili ni kijani-zeituni, mbavu zina rangi ya fedha na mapezi yana kingo nyeusi. Wana miale myororo 13-17 mgongoni, miale myororo 8-10 mkunduni na miale 31 mkiani.

Msambao na makazi

Fupefupe hutokea Bahari ya Hindi na ya Pasifiki kutoka Afrika Kusini mpaka Hawaii na Visiwa vya Markesas, kutoka Kalifornia mpaka Visiwa vya Galapagos, kaskazini mpaka Japani na kusini mpaka Australia. Huishi katika maji ya bahari karibu na pwani ya visiwa na kando ya matako ya mabara, kwa kina cha m 1 hadi 30. Pia mara nyingi huingia ndani ya milango ya mito na mito yenyewe.

Biolojia

Kwa kawaida samaki hawa hujilisha bakteria kijani-buluu, miani na invertebrata wadogo. Huwa kuunda makundi karibu na pwani na visiwa vyenye miamba ya matumbawe. Samaki wachanga hukaa baharini kwa wiki mbili hadi tatu na kisha, wakati wa hatua ya samaki vijana, huhamia nyangwa, milango ya mito na pengine maziwa, na kurudi bahari baadaye ili kukomaa kingono na kuzaa. Majike hutaga usiku hadi mayai milioni 5 katika maji kame ya chumvi.

Picha

Marejeo

  • Rashid Anam & Edoardo Mostarda (2012) Field identification guide for the living marine resources of Kenya. FAO, Rome.
  • Gabriella Bianchi (1985) Field guide to the commercial marine brackish-water species of Tanzania. FAO, Rome.

Viungo vya nje