Mashariki ya Kati
Mashariki ya Kati (kwa Kiingereza Middle East) ni namna ya kutaja sehemu kubwa ya Asia ya Magharibi pamoja na Afrika ya kaskazini-mashariki, hasa Misri.
Kwa kawaida nchi zifuatazo huhesabiwa humo:
- Nchi za Bara Arabu, zikiwa pamoja na Saudia, Yemen, Oman, Falme za Kiarabu, Katar na Kuwait,
- Nchi za Shamu ya kihistoria, zikiwa pamoja na Syria, Lebanon, Israel na Palestina, Yordani
- Iraq
- Uajemi
- Uturuki
- Misri (ambayo iko upande wa Afrika isipokuwa rasi ya Sinai)
Nchi hizo zinatajwa pamoja kwa sababu zina historia ya pamoja na utamaduni wa karibu.
Matatizo ya jina hili
Jina "Mashariki ya Kati" limesambazwa kutokana na kawaida ya Kiingereza na kutafsiriwa katika lugha mbalimbali. Lina matatizo kadhaa yanayotakiwa kujulikana hata tukiendelea kulitumia:
- kuna namna mbalimbali za kutaja nchi za ziada zinazohesabiwa humo au la (kwa mfano: wengine huhesabu pia nchi za Asia ya Kati kama vile Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan n.k.)
- jina ni tamko la Kiulaya: nchi hizi ziko upande wa mashariki kwa mtu aliyeko Ulaya. Kutoka Uswahilini ingekuwa zaidi "Kaskazini ya Kati"
- matumizi ya jina yamebadilika: zamani Kiingereza pamoja na lugha nyingine za Ulaya kilitofautisha kati ya
- "Mashariki ya Karibu" (Near East),
- "Mashariki ya Kati" (Middle East) na
- "Mashariki ya Mbali" (Far East)
kikimaanisha
- a) nchi za Bara Arabu na jirani;
- b) nchi za Uhindi na jirani
- c) nchi za Asia ya Mashariki kama China, Japani.
Lugha mbalimbali za Ulaya Bara kama Kijerumani zinaendelea kutumia majina hayo matatu vile. Pia wataalamu wa historia kwa Kiingereza hupendelea kutofautisha kati ya "Mashariki ya Karibu" na "Mashariki ya Kati".
Historia ya Mashariki ya Kati
Kitovu cha ustaarabu
Nchi zinazoitwa kwa Kiingereza "Mashariki ya Kati" ziko kwenye eneo la dunia ambako watu na tamaduni za Asia, Afrika na Ulaya hukutana.
Ni pia mahali ambako Bahari Hindi na Mediteranea zinakaribiana ambazo zote mbili zilikuwa njia za usafiri wa mbali tangu kale.
Pamoja na mahali pa kubadilishana bidhaa na teknolojia, eneo hili lilikutanisha pia mawazo, falsafa na dini. Hadi leo Mashariki ya Kati ni kitovu cha kiroho cha dini za Uzoroasta, Uyahudi, Ukristo na Uislamu.
Idadi kubwa ya aina za kwanza za ustaarabu duniani zilianza hapa kama vile Mesopotamia (Sumeri, Akkad, Assyria, Babeli) na Misri ya Kale, zikifuatwa na zile za Uajemi, Ugiriki wa Kale, Israeli ya Kale, Finisia na nyingine.
Muhtasari wa historia ya utawala
Eneo lote liliunganishwa mara ya kwanza chini ya Milki ya Ashuru, halafu na milki ya pili ya Babeli iliyofuatwa na milki ya Uajemi na utawala wa Aleksander Mkuu.
Baadaye eneo liligawiwa hasa kati ya milki mbalimbali za Uajemi na Dola la Roma hadi uenezi wa Waarabu Waislamu na kuundwa kwa milki ya khalifa.
Tangu mwaka 1512 Mashariki ya Kati karibu yote ilikuwa chini ya utawala wa Milki ya Osmani hadi Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Ugawaji wa Milki ya Osmani
Mashariki ya Kati ya kisasa ilianza kutokea baada ya vita hiyo. Ufaransa na Ufalme wa Maungano zilishinda Milki ya Osmani zikagawana maeneo yake ya nje ya Uturuki. Ugawaji huu ulithibitishwa na Shirikisho la Mataifa, hivyo maeneo ya Syria, Lebanoni, Palestina (baadaye Israeli na Yordani) na Iraki yalikabidhiwa kwa nchi hizo mbili za Ulaya kama maeneo ya kudhaminiwa kwa masharti ya kuyaandaa maeneo haya kuwa nchi huru baadaye.
Maeneo kadhaa kwenye rasi ya Uarabuni yalibaki huru baada ya kuondoka kwa jeshi la Osmani hadi mwaka 1918:
- Chifu Ibn Saud wa Riyad alishinda vita baina ya makabila ya Uarabuni ya kati akaweza kuvamia na kutawala maeneo ya Najd na Hejaz na mwaka 1932 alitangaza Ufalme wa Uarabuni wa Saudia
- Katika Yemen Imamu Yahya Muhamad wa kundi la Zaidiya alivamia velayat ya Yemen ya Kiosmani na kutangaza Ufalme wa Yemen
Uhuru ulifika kwa ngazi mbalimbali na tofauti kwa kila nchi.
Maeneo ya kudhaminiwa kwa Uingereza:
- Iraki ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Shirikisho la Mataifa mwaka 1932 ingawa hali halisi ilikuwa nchi lindwa chini ya athira ya Uingereza hadi mwaka 1958.
- Palestina ng'ambo ya mto Yordani (Transjordan) ilipata serikali ya kujitawala kama nchi lindwa chini ya Uingereza tangu mwaka 1922, halafu uhuru kamili mwaka 1946 kwa jina la Transjordani, halafu Yordani tu
- Israeli ilikubaliwa na Umoja wa Mataifa kuwa nchi huru mwaka 1948.
- Azimio lilelile lililenga kuanzisha pia dola la Kiarabu la Palestina lakini, kutokana na vita iliyoanza mara moja, hii haikutokea, maeneo yaliyotarajiwa kuwa Palestina yalivamiwa na Israeli, Yordani na Misri. Tangu mwaka 1993 kuna Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina yenye viwango tofauti vya utawala juu ya sehemu za maeneo ya Palestina asilia zilizo chini ya usimamizi wa kijeshi wa Israel.
Maeneo ya kudhaminiwa kwa Ufaransa:
- Lebanoni ilitangaza uhuru wake mwaka 1943 wakati Ufaransa ulikuwa chini ya Ujerumani wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
- Syria ilikuwa huru mwaka 1946.
Maeneo mengine baada ya Vita Kuu ya Kwanza
Katika nchi kadhaa zilizokuwa nje ya Milki ya Osmani Uingereza ilikuwa na athira kubwa na hali halisi nchi hizo zilikuwa nchi lindwa kabla na baada ya Vita Kuu ya Kwanza
- Misri ilikuwa rasmi sehemu ya Milki ya Osmani lakini hali halisi ilisimamiwa na Uingereza hasa kwa shabaha ya kusimamia mfereji wa Suez. Mwaka 1914 ilitangazwa kuwa nchi lindwa chini ya Uingereza; tangazo la uhuru la mwaka 1922 bado liliacha athira kubwa kwa Uingereza. Tangu mwaka 1952 Misri imepata uhuru kamili, na tangu hapo ilitawala pia mfereji wa Suez.
- Omani ilikuwa eneo lililogawiwa kati ya Sultani wa Maskat na Imamu wa Ibadiya mnamo 1890. Maskat ilikubali kuwa eneo lindwa chini ya Uingereza ikapata msaada wa jeshi la Uingereza dhidi ya Saudia na baadaye kuvamia na kutawala pia maeneo ya imamu mwaka 1957. Mkataba wa mwaka 1951 ulitangaza uhuru wa Omani, lakini hali halisi athira ya Uingereza ulikuwa na nguvu hadi miaka ya 1990.
- Kuwait ilikuwa nchi lindwa chini ya Uingereza tangu mwaka 1899 na Waingereza walitetea hali yake ya pekee dhidi ya Waosmani na baadaye dhidi ya Saudia. Ilipata uhuru mwaka 1961.
- Maeneo ya Falme za Kiarabu pamoja na Qatar na Bahrain yalikuwa nyumbani kwa makabila madogo na chifu zao. Tangu mwaka 1820 walikuwa na mikataba na Uingereza walipoahidi kuachana na uharamia na kupokea ulinzi wa Uingereza. Ulinzi huu ulizuia uvamizi wa Saudia katika karne ya 20. Tangu mwaka 1971 madola hayo madogo yalipata uhuru. Saba kati yake yaliungana kuwa Falme za Kiarabu.
Ugunduzi wa mafuta
Hadi Vita Kuu ya Kwanza mataifa yote katika eneo la Ghuba ya Uajemi yalikuwa dhaifu, bila uchumi imara na bila uwezo wa kijeshi. Hasa upande wa Uarabuni watawala wadogo walisimamia miji michache kwenye pwani tu na sehemu kubwa ya watu waliishi katika utaratibu wa kikabila bila kujali serikali.
Kugunduliwa mafuta kulibadilisha hali hii katika miaka baada ya vita. Mafuta ya petroli yaligunduliwa mwaka 1908 katika Iran kusini na serikali ya Uingereza ilinunua mara moja hisa nyingi za kampuni ya Anglo-Persian Oil iliyokuwa na mkataba wa kuzalisha mafuta huko.
Vita kuu ya kwanza ya dunia ilionyesha kwa mara ya kwanza umuhimu wa kijeshi ya mafuta.[1].
Mafuta yalibadilisha umuhimu wa Mashariki ya Kati. Mafuta ya petroli yaliendelea kuwa chanzo muhimu zaidi cha nishati katika uchumi wa dunia ya kisasa. Kwa hiyo mataifa na makumpuni makubwa yalianza kuangalia hali ya kisasa ya nchi zenye mafuta. Yalijaribu kuhakikisha ya kwamba wawepo watawala na serikali ambao wawape nafasi nzuri na nafuu ya kupata mafuta kutoka ardhi yao. Vilevile yalijaribu kuzuia nchi nyingine kuingia huko.
Mashindano hayo yaliweka msingi kwa siasa ya nchi hizo za Kiarabu, ambazo zote zilikuwa na watu wachache lakini mafuta mengi, kuwa chini ya athira za nje ilhali mataifa makubwa yalihakikisha kuwepo kwao na mapato makubwa kwa watawala, hivyo pia kuwalinda dhidi ya mabadiliko ya kisiasa na kimapinduzi yaliyoonekana katika nchi nyingine za Mashariki ya Kati zisizo na utajiri wa mafuta.
Nchi ya kwanza iliyopata nafasi ilikuwa Uingereza ikifuatwa na Marekani. Mwaka 1932 kampuni ya Standard Oil ya Kalifornia ikakuta mafuta huko Bahrain ikaendelea kujipatia leseni ya kuyatafuta pia Saudia wakafaulu mwaka 1938.
Utajiri haukuanza kote mara moja; Uajemi (Iran) ilikuwa nchi kubwa ikapata asilimia ndogo ya mapato ya mafuta kufuatana na mikataba ya zamani; upande wa Uarabuni ilichukua muda hadi chemchemi kubwa za mafuta zilipatikana na kuzalisha kwa wingi. Bahrain ilitangulia, Kuwait ilifuata tangu mwaka 1950 hivi, lakini Omani na Falme za Kiarabu zilianza kuzalisha kwa wingi katika miaka ya 1970 pekee.
Mwanzoni uchumi wa mafuta ulikuwa kabisa mikononi mwa makampuni ya nje kwa sababu wenyeji hawakuwa na elimu ya teknolojia na watawala walikosa mapato mengine, hivyo walikubali masharti yoyote. Tangu miaka ya 1960 polepole asilimia ya mapato iliyobaki mikononi mwa serikali iliongezeka, pia zilianza kununua hisa za makampuni yaliyozalisha mafuta katika ardhi yao.
Hadi miaka ya 1990 serikali za nchi za ghuba zilikuwa na hisa nyingi katika makampuni haya yaliyokuwa sasa mali ya taifa au ya familia tajiri za wenyeji.
Mapato kutokana na mafuta yalianza kubadilisha maisha na jamii za nchi zote zinazouza mafuta kwenye soko la dunia. Hasa watawala wa nchi ndogo walikuwa matajiri kupita kiasi, wakaweza kuendelea na mfumo wa utawala wa mfalme asiyebanwa na katiba kwa muda mrefu kwa sababu waliweza kuwagawia wananchi wao sehemu za utajiri wa mafuta.
Wakati wa vita baridi mashindano kati ya magharibi na Umoja wa Kisovyeti yaliendeshwa vikali katika Mashariki ya Kati. Serikali mbalimbali zilichezacheza kati ya pande hizo mbili.
Wakazi
Leo hii wakazi wa Mashariki ya kati mara nyingi wanatazamwa kwa jumla kuwa "Waarabu". Hii ni kweli kwa kiasi tu kwa sababu mbili
- Nchi kadhaa kama Uturuki, Iran na Israel zina wakazi Waarabu wachache tu
- Kwa jumla eneo hili ni mchanganyiko mkubwa wa makabila mengi na vikundi vingi vyenye lugha, tamaduni na dini tofautitofauti, wakiwemo wahamiaji wengi sana, pengine kuliko wananchi wenyewe.
Ni kweli kwamba idadi kubwa ya wakazi leo hii wanatumia lugha ya Kiarabu. Lugha muhimu katika eneo hili ni:
- Kiarabu
- Kifarsi (pamoja na lugha za Kiirani mbalimbali)
- Kituruki (pamoja na lugha za Kiturki mbalimbali)
- Kiberber
- Kikurdi
pamoja na lugha nyingine mbalimbali kama Kiebrania, Kiaramu, Kiarmenia na lugha asili za wahamiaji.
Picha za Miji ya MAshariki ya Kati
-
Abu Dhabi - Falme Arabu (UAE)
-
Ankara - Uturuki
-
Baghdad - Iraq
-
Beirut - Lebanon
-
Kairo - Misri
-
Dameski - Syria
-
Doha - Qatar
-
Dubai - UAE
-
Istanbul - Uturuki
-
Yerusalemu (Israeli-Palestina)
-
Kuwait City - Kuwait
-
Manama - Bahrain
-
Mekka - Saudi Arabia
-
Ramallah - Palestina
-
Sana'a - Yemen
-
Tabriz - Iran
-
Tehran - Iran
-
Tel Aviv - Israel
Tanbihi
Viungo vya nje
Makala hii kuhusu eneo fulani bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Je, unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.
|