Msalaba wa Yesu
Msalaba wa Yesu ni msalaba ule ambao Yesu Kristo alisulubiwa juu yake hadi kifo chake kilichotokea huko Yerusalemu kwa amri ya Ponsyo Pilato siku ya Ijumaa, labda tarehe 7 Aprili 30 BK.
Tukio hilo, pamoja na ufufuko wa Yesu unaosadikiwa na Ukristo kutokea siku ya tatu (Jumapili ya Pasaka), ndiyo kiini cha imani ya dini hiyo mpya iliyotokana na ile ya Uyahudi.
Kwa Wakristo fumbo hilo la Pasaka ndilo kilele cha historia ya wokovu inayotangazwa na Biblia ya Kikristo.
Fumbo hilo lilisababisha kazi nyingi za sanaa ya Kikristo, hasa uchoraji na uchongaji.
Historia
Adhabu hiyo kali ilianza kutumika huko Uajemi na kuenea hadi Dola la Roma ambalo liliitumia hasa katika maeneo ya pembeni na kwa watumwa.
Kadiri ya Injili zote nne, Ponsyo Pilato, liwali wa Palestina (26-36), aliamua Yesu aadhibiwe hivyo kulingana na shtaka la viongozi wa Wayahudi waliodai kwamba mtuhumiwa alijitangaza kuwa mfalme na kupinga mamlaka ya Kaisari wa Roma, kwa wakati huo Tiberius, ingawa Pilato alikuwa ametambua shtaka halikuwa la kweli, bali lilitokana na husuda.
Kadiri ya Injili ya Yohane, Pilato mwenyewe alisisitiza kwamba, katika maandishi yaliyotakiwa kuwajulisha watu sababu ya adhabu hiyo, iwekwe wazi kwamba Yesu aliuawa kama mfalme wa Wayahudi, ingawa neno hilo lilichukiza viongozi wa taifa.
Maneno ya ilani hiyo yaliandikwa katika lugha tatu:
- Kilatini: Iesus Nazarenus Rex Iudeorum, kifupi INRI,
- Kigiriki: Ἰησοῦς ὁ Ναζωραῖος ὁ Bασιλεὺς τῶν Ἰουδαίω. Kutokana na herufi hizo, Wagiriki wanaandika INBI.
- Kiebrania: ישוע הנוצרי ומלך היהודים. Herufi za kwanza za maneno hayo kwa Kiebrania ni יהוה, YHWH, ndilo jina takatifu la Mungu katika Biblia ya Kiebrania.
Yesu akiwa msalabani alisema maneno kadhaa. Kati ya hayo, ni maarufu maneno saba yaliyoripotiwa na Injili yakimuelekea Mungu Baba, Bikira Maria, Mtume Yohane na mhalifu aliyesulubiwa pamoja naye.
Tazama pia
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Msalaba wa Yesu kama historia yake, matokeo au athari zake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |