Gesi adimu
Gesi adimu ni mfulizo wa kikemia katika mfumo radidia unaounganisha elementi za kundi la 18 yaani Heli (He), Neoni (Ne), Arigoni (Ar), Kriptoni (Kr), Xenoni (Xe) na Radoni (Rn).
Elementi hizi zote zapatikana kama gesi kwa hali sanifu; hazina rangi wala harufu; haziwaki.
Zinapatikana katika hali ya atomu pekee, si kama molekyuli. Hazimenyuki yaani haziungani na atomu yingine kuwa molekyuli. Sababu ya kutomenyuka ni tabia ya mzingo elektroni wa nje kujaa kabisa; hapa mzingo elektroni wa nje huwa na idadi ya elektroni inayowezekana tofauti na elementi nyingi ambako mzingo elektroni wa nje ina idadi ya elektroni ambayo ni chini ya idadi ya nafasi zake. Kwa hiyo hakuna haja kutafuta hali thabiti zaidi; gesi hizi zimeshafikia hali thabibiti kila atomi peke yake. Hivyo hakuna kampaundi za gesi hizi.
Gesi hizi zote ziko hewani lakini kwa kiasi kidogo tu. Radoni pekee yake ni hatari ya binadamu lakini si kwa sababu ya tabia zake za kikemia bali na tabia yake ya kifizikia kwa sababu radi ni elementi mnururishi.